MASHITAKA 11 dhidi ya aliyekuwa Naibu Katibu Mkuu wa Chadema, Zitto Kabwe, yamebainisha kuwa kosa kubwa la kiongozi huyo kijana, ni nia yake ya kutaka kuwania nafasi ya Mwenyekiti wa Taifa, Freeman Mbowe.
Chanzo chetu cha habari kilichoona mashitaka hayo kabla ya kutumwa kwa washitakiwa, kimebainisha kuwa makosa saba kati ya makosa 11, yanahusu kugombea uenyekiti Taifa, au kumkashifu Mwenyekiti wa Taifa.
“Ukiona hayo mashitaka yenyewe ndugu yangu, yanajirudia rudia na kuzunguka katika kosa moja la nia ya kuwania nafasi ya Mwenyekiti wa Taifa… angalia kosa la kwanza, kosa la tatu, tano, sita nane na tisa, ni kama vile kuwania uenyekiti ndio kosa kubwa.
“Hata hivyo kwa jinsi mgawanyiko ulivyo ndani ya chama sasa, nakuhakikishia hawa jamaa (Zitto, Dk Kitila Mkumbo na Samson Mwigamba), watarudishwa katika nyadhifa zao na hakuna atakayeadhibiwa,” alisema mtoa taarifa wetu.
Alinukuu kauli ya Mjumbe wa Kamati Kuu ya Chadema, Profesa Mwesiga Baregu aliyehoji kama makosa wanayotuhumiwa akina Zitto ni makubwa kiasi cha kuyeyusha mema aliyoyafanya katika chama. “Si umesikia akina Baregu wakizungumza? Kwa mashitaka yale nakuhakikishia kitakachofanyika ni kufunika kombe mwanaharamu apite,” alisema mtoa habari wetu.
Kosa la kwanza kwa Zitto, Dk Mkumbo na Mwigamba, wanadaiwa kuvunja Kanuni ya Chama inayokataza kukashifu chama, kiongozi au mwanachama yeyote. Katika maelezo ya kosa hilo, akina Zitto wanadaiwa kumkashifu Mwenyekiti wa Taifa, Mbowe, Katibu Mkuu, Dk Willibrod Slaa na Mjumbe wa Kamati Kuu, Godbless Lema.
Moja ya madai katika mashitaka hayo, ni kilichoandikwa katika Mkakati wa Mabadiliko 2013, kuwa Mbowe amekuwa akinunua vifaa vyote vya chama nje ya nchi kwa bei anayoijua mwenyewe na ambayo haihojiwi popote. Wanadaiwa pia wamemkashifu Dk Slaa kwa kudai ni mdhaifu kwa kumruhusu Mbowe kuingilia shughuli za kiutendaji.
Zitto na wenzake wanadaiwa katika kosa la pili, kutokuwa wawazi na wa kweli wakati wote na kushirikiana na vikundi vya majungu na udanganyifu kinyume na Kanuni za Uendeshaji kipengele cha 10.1 (VIII.
Katika kosa la tatu, wanadaiwa kutoa tuhuma juu ya viongozi wenzao bila kupitia vikao halali na utaratibu wa ngazi zilizowekwa, kinyume na kanuni ya 10.1 (X).
Katika kosa la nne, akina Zitto wanadaiwa kujihusisha na vikundi vyenye misingi ya ukabila, udini au ukanda ambavyo vina makusudi ya kubaguana ndani ya chama, miongoni mwa jamii, kisiasa au kijamii. Katika kosa hilo wanadaiwa kwenda kinyume na kipengele cha 10.1 (IV), cha Kanuni za Uendeshaji wa Chama.
Akina Zitto katika kosa la tano, wanadaiwa kujihusisha na vitendo vya kuchonganisha na kuzua migogoro kwa viongozi wa chama au wanachama, kinyume na kifungu cha 10.1 (IX), cha Kanuni za Uendeshaji wa Chama.
Katika kosa la sita ambalo mtoa habari wetu alisema ndio kubwa, Zitto na wenzake wanadaiwa kutekeleza mpango wa kusudio la kugombea uenyekiti wa Chama Taifa, bila kutangaza kusudio la kutangaza nafasi hiyo.
Hatua hiyo inadaiwa kuwa ni kinyume na kifungu 2.C cha Muongozo wa Kutangaza Kusudio la Kuwania Nafasi ya Uongozi wa Chama, Mabaraza na Serikali wa 2012.
Zitto na wenzake katika kosa la saba, wanadaiwa kutengeneza mitandao ya kuwania uongozi ndani ya chama kwa nia ya kujihakikishia ushindi kinyume na kanuni ya 2 (D), ya Muongozo wa Kuwania Uongozi.
Katika kosa la nane, Zitto na wenzake wanadaiwa kuwachafua viongozi na wanachama wengine wenye kusudio/nia ya kutaka kugombea nafasi ya uenyekiti kinyume na kifungu 2 (E) cha Muongozo wa Kuwania Uongozi.
Katika kosa hilo, kumewekwa maelezo ya ziada kuwa kosa hilo linaunganishwa na kosa la kwanza ambalo washitakiwa wanadiwa kuwakashifu Mbowe, Dk Slaa na Lema.
Kosa la tisa, akina Zitto wanadaiwa kujihusisha na upinzani dhidi ya chama na makundi ya majungu ya kugonganisha viongozi na wanachama wakati wa uchaguzi wa chama, kinyume na kifungu cha 10.3 (IV), cha Kanuni za Uendeshaji.
Kosa la kumi linamhusu Zitto peke yake, ambapo anaidaiwa kukashifu chama na kiongozi wa chama nje ya Bunge kinyume na kifungu 2 C (B), kikisomwa pamoja na kifungu 3 B cha Kanuni za Mwenendo wa Maadili ya Wabunge.
Katika hilo Zitto kwa kushirikiana na baadhi ya viongozi wa chama yaani Dk Mkumbo na Mwigamba na mtu mwingine ambaye hajajulikana, wanadaiwa kusambaza waraka uitwao Mkakati wa Mabadiliko 2013.
Mkakati huo, unadaiwa kukashifu chama na/ au viongozi wake wakuu kama ilivyoelezwa katika kosa la kwanza, tatu, nne na nane.
Mwisho katika kosa la 11, Zitto na wenzake wanadaiwa kuchochea mgawanyiko ndani ya chama kinyume na kanuni ya 3 F ya Kanuni za Mwenendo wa Maadili ya Bunge.
No comments:
Post a Comment