Rais wa Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete ametaka wananchi wa Kenya
wapewe nafasi ya kuamua ni viongozi gani wanawataka katika Uchaguzi Mkuu
uliopangwa kufanyika Machi mwakani.
Aidha,
Rais Kikwete amesema kuwa wananchi wa Kenya wanayo haki ya msingi kabisa kuamua
hatma ya taifa lao katika Uchaguzi Mkuu huo.
Mheshimiwa
Rais ameyasema hayo jana Oktoba 21, 2012 alipokutana na kufanya mazungumzo na ujumbe
wa wabunge wa vyama mbalimbali vya siasa vya nchini Kenya uliomtembelea Ikulu
jijini Dar es salaam.
Ujumbe huo
uliongozwa na Naibu Waziri Mkuu wa Kenya na Waziri wa Fedha Mhe. Uhuru Kenyatta
ambaye pia ni Mwenyekiti wa chama cha TNA na Waziri wa Sheria wa Kenya
Mhe Eugene Wamalwa wa chama cha New Ford Kenya. Wote wawili ni wagombea wa
nafasi ya Urais katika uchaguzi ujao.
Wengine
katika msafara huo walikuwa ni Naibu Waziri wa Afya na mbunge wa Mombasa Mhe.
Kambi Kazungu, Mbunge wa kuteuliwa wa chama cha TNA Bi Rachel Shebesh, na
Mbunge wa Kajiado kwa tiketi ya TNA Moses ole Sakuda na mbunge wa zamani Mhe
Abdullahi Alli.
Rais
Kikwete aliwapongeza kwa kuamua kufanya kazi kwa pamoja licha ya kuwa
watakuwa washindani katika kinyang’anyiro cha uchaguzi mkuu huo.
Mheshimiwa
Rais ameitakia heri nchi ya Kenya katika uchaguzi huo ujao, na kusisitiza
kwamba nchi hiyo ya jirani ina umuhimu katika mustakabali wa kiuchumi kwa
nchi za Afrika Mashariki.
Rais
Kikwete wakati huo akiwa Mwenyekiti wa Umoja wa Afrika (AU) alikuwa miongoni
mwa viongozi walioshughulika sana kutafuta ufumbuzi wa ghasia na vurugu
zilizozuka kufuatia Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2007 nchini Kenya.
No comments:
Post a Comment