Taifa Stars imetolewa kwenye mechi za mchujo za
Kombe la Mataifa ya Afrika baada ya kufungwa kwa penalti na wenyeji Msumbiji
(The Mambas) katika mchezo uliofanyika Uwanja wa Taifa ulioko Zimpeto pembeni
kidogo ya Jiji la Maputo.
Refa Bennett Daniel
alipopuliza filimbi ya kumaliza dakika 90 za pambano hilo timu hizo zilikuwa zimefungana bao 1-1,
hivyo kwa mujibu wa kanuni za mashindano hayo yanayoandaliwa na Shirikisho la
Mpira wa Miguu Afrika (CAF) mikwaju ya penalti ikatumika kupata mshindi. Katika mechi ya kwanza iliyochezwa Dar es
Salaam, Februari 29 mwaka huu timu hizo zilitoka sare ya bao 1-1. Msumbiji
ndiyo walioanza kupata bao dakika ya 9 lililofungwa na mshambuliaji Jeremias
Sitoe akiungnisha krosi ya Elias Pelembe ambaye mabeki wa Taifa Stars
walifikiri ameotea.
Stars ilisawazisha bao hilo dakika ya 89
likifungwa kwa kichwa na
Aggrey Morris kutokana na
mpira wa kona uliopigwa Amir Maftah. Mikwaju ya penalti tano tano walioifungia
Stars walikuwa Amir Maftah, Shabani Nditi na Shomari Kapombe wakati Aggrey
Morris na Kevin Yondani. Kwa vile The Mambas nao walikosa mbili ikabidi
iongezwe penalti moja moja. Waliofunga kwa upande wa Stars walikuwa John Bocco,
Frank Domayo na Mrisho Ngassa wakati Mbwana Samata alikosa.
Akizungumzia pambano hilo, Kocha wa Taifa
Stars, Kim Poulsen aliwapongeza wachezaji wake kwa kupambana hadi dakika ya
mwisho. Taifa Stars itarejea nyumbani Juni 19 mwaka huu, ambapo itaaondoka hapa
saa 4.40 asubuhi kwa kupitia Nairobi, Kenya na kutua Uwanja wa Ndege wa
Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA) saa 1.50 usiku.
Kikosi kilipangwa hivi;
Juma Kaseja, Shomari Kapombe, Erasto Nyoni/John Bocco, Aggrey Morris, Kevin
Yondani, Shaabani Nditi, Mrisho Ngasa, Frank Domayo, Thomas Ulimwengu/Haruna
Moshi, Mbwana Samata na Mwinyi Kazimoto/Amir Maftah.
No comments:
Post a Comment