YANGA SC
leo imezinduka baada ya kupata ushindi wa mabao 3-1 katika mfululizo wa Ligi
Kuu ya Vodacom Tanzania Bara, dhidi ya wenyeji Toto African, kwenye Uwanja wa
CCM Kirumba mjini Mwanza.
Matokeo
haya, yanaifanya Yanga itimize pointi 11, katika mechi saba ilizocheza hadi
sasa, ikiwa imefungwa mbili, sare mbili na kushinda tatu, inazidiwa pointi tano
na wapinzani wake wa jadi, Simba SC wanaoongoza ligi hiyo kwa pointi zao 16,
wakifuatiwa na Azam wenye pointi 13.
Hadi
mapumziko, Yanga walikuwa tayari mbele kwa mabao 2-0, yaliyopachikwa kimiani na
mshambuliaji wa kimataifa wa Burundi, Didier Kavumbangu na beki wa kimataifa wa
Rwanda, mwenye asili ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC), Mbuyu Twite.
Kavumbangu
alifunga bao la kwanza dakika ya pili, baada ya kuuwahi mpira uliotemwa na kipa
Erick Ngwengwe kufuatia kona iliyochongwa na Haruna Niyonzima, hilo likiwa bao
lake la tano ndani ya mechi 11 tangu ajiunge na Yanga msimu huu akitokea
Atletico ya kwao, Burundi.
Baada ya
bao hilo, Yanga waliendelea kulisakama lango la Toto na dakika ya 21, Mbuyu
Twite akaunganisha kona ya chini chini iliyochongwa na Niyonzima.
Toto
ilipoteza nafasi nzuri ya kufunga dakika ya 42, baada ya kupata penalti,
kufuatia beki mmoja wa Yanga kuunawa mpira kwenye eneo la hatari, baada ya Wana
Kishamapanda kufanya shambulizi kali la kushitukiza, lakini kiungo Emanuel
Swita akapiga nje.
Swita
alipiga penalti nzuri tu ya chini pembeni kabisa, lakini vipimo vyake vikazidi
kidogo, mpira ukatoka nje, ingawa Berko aliifuata vizuri pembeni kabisa kulia
kwake na angeweza kuokoa.
Kipindi
cha pili Toto waliingia kwa kasi zaidi na kuanza kulishambulia lango la Yanga
mfululizo, wakitawala zaidi sehemu ya kiungo.
Katika
dakika ya 54 mshambuliaji Mussa Said aliifungia Toto bao safi, baada ya kipa
Yaw Berko kutoka langoni.
Baada ya
bao hilo, Toto walizidi kutawala mchezo na kukosa mabao mawili ya wazi- hapo
ndipo kocha Mholanzi, Ernie Brandts akawatoa viungo Frank Domayo na Athumani
Idii ‘Chuji’ na kuwaingiza Shamte Ally na David Luhende.
Walipoingia
Shamte na Luhende wote walienda kushambulia pembeni na Haruna Niyonzima na
Nurdin Bakari wakarudi katikati.
Mabadiliko
hayo yaliisaidia Yanga kupata bao la tatu dakika ya 68, lililofungwa kitaalamu
na mshambuliaji Jerry Tegete ambaye alimpiga chenga kipa Ngwengwe baada ya
kupokea pasi ya Oscar Joshua.
Baada ya
bao hilo, Kocha wa Toto, Johh Tegete naye alifanya mabadiliko akiwatoa Mussa
Said na Evarist Maganga na kuwaingiza Heri Mohamed na Heri Kyaruzi. Hata hivyo,
pamoja na mabadiliko hayo, Yanga waliendelea kutawala mchezo hadi filimbi ya
mwisho.
Kwa
ushindi huu, Yanga imelipa kisasi cha mara ya mwisho timu hizo, zilipokutana
kwenye Uwanja huo, Jumapili ya Aprili 15, mwaka huu, Toto walipoibuka na
ushindi wa mabao 3-2.
Katika
mchezo huo, kikosi cha Yanga kilikuwa;
Yaw
Berko, Juma Abdul, Oscar Joshua, Nadir Haroub ‘Cannavaro’, Mbuyu Twite,
Athumani Iddi ‘Chuji’/Shamte Ally, Frank Domayo/David Luhende, Haruna
Niyonzima, Jerry Tegete, Didier Kavumbangu na Nurdin Bakari.
No comments:
Post a Comment