Mahakama
moja ya Iraq imewahukumu adhabu ya kifo Tariq al Hashimi Makamu wa Rais wa nchi
hiyo aliyeikimbia nchi na msaidizi wake kwa kuhusika katika vitendo vya kigaidi
na kuendesha kikosi cha mauaji.
Hashimi anatuhumiwa kuhusika
katika mashambulizi ya mabomu dhidi ya serikali na maafisa wa usalama wa nchi
hiyo miaka kadhaa iliyopita likiwemo shambulio la bomu lililotegwa kwenye gari
lililotekelezwa mwezi Novemba mwaka jana huko Baghdad mji mkuu wa Iraq ambalo
lilikuwa limekusudia kumlenga Waziri Mkuu wa nchi hiyo. Tarehe 19 Disemba mwaka
jana kamati ya uchunguzi kutoka Wizara ya Mambo ya Ndani ya Iraq ilitoa waranti
wa kumtia mbaroni Tariq al Hashimi baada ya walinzi wake watatu kukiri kuwa
walikuwa wakiamuriwa na Makamu huyo wa Rais wa Iraq kutekeleza mashambulio ya
kigaidi. Hata hivyo al Hashimi baadae alikimbilia huko Kurdistan.
No comments:
Post a Comment