Kaimu Mkurugenzi Mtendaji mpya wa Shirika la Ndege la Air Tanzania (ATCL), Kapteni Milton Lusajo Lazaro.
---
Na Mwandishi wetu
IKIWA ni siku mmoja tu
baada ya kuteuliwa kuwa Kaimu Mkurugenzi Mtendaji mpya wa Shirika la
Ndege la Air Tanzania (ATCL), Kapteni Milton Lusajo Lazaro amesema
shirika hilo linanafasi kubwa ya kupata mafanikio iwapo litaendelea
kutekeleza mpango wake wa maendeleo wa miaka mitano.
Kwa mujibu wa taarifa
iliyotolewa jana, Lusajo alisema atatumia uzoefu wake alioupata katika
sekta ya usafiri wa anga kuleta mabadiliko katika shirika hilo na
kuliwezesha kushindana sambamba na kampuni nyingine za ndani na nje ya
nchi.
Kpt. Lusajo, rubani
anaeheshimika katika sekta ya usafiri wa anga si kwa Afrika Mashariki
pekee ila Afrika kwa ujumla ana rekodi ya kuendesha ndege kwa saa zaidi
ya elfu kumi na mbili, pia amewahi kushika nyadhifa mbali mbali katika
Mamlaka ya Usafiri wa Anga Tanzania (TCAA) pamoja na ATCL kabla ya
kuteuliwa kuwa Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa ATCL.
“Napenda
kutoa shukrani zangu kwa Waziri Mwakyembe na viongozi wengine wa Wizara
kwa kuwa na imani nami. Nimekubali uteuzi wake na nitafanya kazi
aliyonipa kwa moyo mmoja.
Ninaahidi kuwa
nitautumia uzoefu wangu wa zaidi ya miaka 35 katika sekta ya usafiri wa
anga na kuipa ATCL uwezo kushindana kibiashara. Natoa wito kwa
wafanyakazi wenzangu kutoa ushirikiano ili tuweze kusonga mbele. ”
Alisema.
Lazaro alisema Shirika lake
litaendelea kutoa huduma kama kawaida na kuongeza kuwa safari zote za
Shirika zitaendelea kama ilivyopangwa na ratiba licha ya mabadiliko ya
uongozi.
“Hakuna sababu ya wananchi
kuwa na wasi wasi. Kilichotokea ni mabadiliko ya uongozi tu lakini
mipango na shughuli zote za Shirika zinaendelea kama ilivyopangwa,”
alisema.
Lazaro aliongeza kusema,
kuwa jukumu kubwa alionalo mbele yake ni kuongeza idadi ya ndege za
shirika hilo aidha kwa kukodi au kuingia ubia na mashirika mengine
katika jitihada za kuimarisha nafasi ya kampuni yake ili iweze
kushindana Kitaifa na Kimataifa katika miaka michache ijayo.
“ATCL haiwezi
kupata mafanikio bila kuwa na ushirikiano mzuri na Serikali pamoja na
wananchi kwa ujumla. Nawaomba wananchi waendelee kuonyesha ushirikiano
na uzalendo waliouonyesha katika wiki chache zilizopita baada ya kuanza
kwa huduma za kampuni yetu.
“Nawahakikishia wateja wetu
na wananchi kwa ujumla kuwa kampuni yangu itaendelea kutoa huduma na
bidhaa bora zilizo katika bei za kiushindani ukilinganisha na makampuni
mengine yanayotoa huduma hii katika soko,” alisema.
No comments:
Post a Comment