BAADHI YA WANANCHI WAKISHANGAA BAADA YA FAINES KUZINDULIWA NA MTOTO MWENYE MIAKA KUMI ALIYEKABIDHIWA MIKOBA NA MAMA YAKE.
BIBI NA MJUKUU WAKE WANAOSADIKIWA NI WACHAWI WAKIWA KATIKA GARI LA POLISI.
FAINES AKIPAKIWA KATIKA GARI YA POLISI.
FAINES ZAWADI-BINTI ALIYEFARIKI KWA MUDA NA KUREJESHWA DUNIANI AKIWA AMESHIKILIWA NA NDUGU ZAKE.
Jeshi la Polisi mkoani Kigoma limefanikiwa kuwaokoa watu watatu
waliokuwa wamezingirwa na kundi la wananchi wakitaka kuwaua kwa tuhuma
za kujihusisha na vitendo vya ushirikina.
Kaimu Kamanda wa Polisi Mkoani Kigoma SSP Joseph Konyo, aliwataja
watu hao waliokolewa kuwa ni Evania Sephanga(50), mkazi wa wilaya ya
Kibondo, Bruno January(46), mkazi wa kijiji cha Nyamhoza na mtoto mmoja
mwenye umri wa miaka kumi na mkazi wa kijiji cha Nyamhoza Kigoma mjini
ambaye jina lake linahifadhiwa.
Kamanda Konyo amesema kuwa wiki iliyopita majira ya saa tisa
mchana, watu hao walizingirwa na kundi hilo kwa madai kuwa walimroga na
kumuua msichana mmoja aitwaye Faines Zawadi(20) mkazi wa kijiji hicho
cha Nyamhoza ambaye siku moja kabla ya kifo chake alionekana kama mtu
aliyechanganyikiwa na kuwa kama kichaa.
Alisema katika tukio hilo, bibi kizee mmoja ambaye alikuwa
mshirika wa kundi la waliodaiwa kuwa wachawi, alifanikiwa kutoroka
katika mazingira ya kutatanisha alipojifanya kuwa anakwenda kujisaidia.
Kamanda Konyo amemtaja bibi huyo aliyefanikiwa kutoroka kuwa ni
Bibi Editha Dosiyo mkazi wa kijiji hicho ambaye baadaye alipatikana na
kuhojiwa kabla ya kukabidhiwa kwa Idara ya ustawi wa jamii baada ya
kuonekana kuwa maisha yake yangekuwa hatarini.
Amesema baada ya Polisi kupata taarifa za tukio hilo, walikimbia
na kwenda kuwaokoa kutoka katika mikono ya kundi la wananchi lakini
wakiwa wameshaadhibu ingawa ilikuwa haijawa kwa kiasi kikubwa.
Habari zinasema kuwa, baadhi ya wananchi walipata taarifa kutoka
kwa mtoto aliyeokolewa akisema kuwa baadhi ya watoto waliofariki
kijijini hapo, akiwataja (majina tunayahifadhi) alikuwa akiwaona
nyumbani kwao nyakati za usiku wakiosha vyombo na baadaye kupewa
chakula.
Siku ya tukio hilo, baadhi ya wananchi walisema kuwa kabla ya bibi
huyo kutoweka alimnong’oneza jambo mjukuu wake ili amfanyie mareheme
ikiwa ni pamoja na kumruka mara saba kisha bibi huyo alitoweka
akijifanya anakwenda kujisaidia.
Walisema mara baada ya bibi huyo kutoweka, mtoto huyo wa kiume
ambaye ni miongoni mwa waliozingirwa wakitaka kuuawa, aliamza kutekeleza
maagizo ya bibi huyo na alipomaliza kitendo cha kumruka kwa mara ya
saba, msichana yuyo ambaye alikuwa ni marehemu alizinduka na kuomba uji.
Wamesema msichana huyo ambaye alikuwa mfu, alipewa uji na kunywa
kisha akapelekwa hospitalini ambako hadi sasa hali yake inasemekana kuwa
inaendelea vizuri.
Hata hivyo Kamanda Konyo ametoa wito kwa wananchi kuacha kuchukua
sheria mkononi na badala yake watoe taarifa Polisi kwa kila jambo
wanaloliona kuwa linaweza kuleta uvunjifu wa amani ili hatua za haraka
zichukuliwe dhidi ya wahusika.
Mwezi uliopita watu wawili mke na mume, waliuawa na kundi la watu
wenye hasira kisha miili yao kuchomwa kwa moto mkoani Kigoma baada wa
kutuhumiwa kuwa walikuwa ni wachawi.
No comments:
Post a Comment