BIASHARA ya dawa za kulevya
imeshika kasi mkoani Iringa huku vigogo kadhaa wakitajwa kuhusika,
Kwanza Jamii-Iringa linaripoti.
Taarifa zinaeleza kwamba,
wafanyabiashara kadhaa maarufu mkoani humo wanatajwa kujihusisha katika
usambazaji na utumiaji wa dawa hizo, hususan cocaine, heroin na Mandrax.
Kundi rika la vijana wenye umri
kati ya miaka 18 na 35 ndilo linaloongoza kwa biashara hiyo kwa utumiaji
na usambazaji, huku bhangi ikiwa inaongoza miongoni mwa orodha ya dawa
za kulevya.
“Huwezi kuipiga vita biashara ya dawa za
kulevya ikiwa vigogo wenyewe ndio wanaosambaza na kutumia. Wapo
wanajulikana, lakini hatujui ni kwa vipi serikali inashindwa
kuwakamata,” kimeeleza chanzo chetu cha habari.
Inaelezwa kuwa, wafanyabiashara kadhaa
wa mjini humo, ambao baadhi wanadaiwa kuwemo kwenye orodha ya vigogo 58
wa dawa za kulevya iliyopelekwa kwa Rais Jakaya Kikwete mwaka 2006, ndio
miungu-watu wanaojificha kwenye mwavuli wa biashara zao halali pamoja
na kusaidia jamii.
Taarifa zinaeleza kwamba, vigogo
wengi na hasa wenye fedha, ndio watumiaji wakubwa wa dawa za viwandani
kama heroin na cocaine kwa vile hawawezi kwenda kununua bhangi mitaani
kutokana na hadhi zao, huku kundi kubwa la vijana likitajwa kutumia
zaidi bhangi.
Wananchi kadhaa waliohojiwa na gazeti
hili kwa masharti ya kutotajwa majina yao, walisema matumizi ya dawa za
kulevya mkoani humo yanazidi kushika kasi licha ya serikali kusema
yamepungua.
“Huku mitaani sisi ndio
tunaowaona watumiaji, wanaongezeka kila wakati na hakuna juhudi za
kuwapunguza, hasa vijana ambao wanazidi kuathirika na matumizi hayo,”
walisema wananchi hao.
Kauli hiyo ya kukithiri kwa matumizi ya
dawa za kulevya iliungwa mkono na Ofisa Mtendaji wa Kata ya Kitanzini
iliyo katikati ya Manispaa ya Iringa, Raphael Magata, ambaye alisema
matumizi ya dawa za kulevya kwa vijana yanazidi kuongezeka.
Magata alisema kwamba, pamoja na juhudi
kubwa zinazofanywa na serikali pamoja na asasi mbalimbali za kijamii
kuelimisha juu ya madhara yake, lakini idadi ya vijana wanaojihusisha na
biashara hiyo inazidi kuongezeka, hivyo kuitaka jamii ishiriki
kupambana ili kuokoa nguvu kazi isipotee.
“Vijana wengi hivi sasa wanajihusisha na
utumiaji wa dawa za kulevya ingawa serikali inajitahidi kuwalimisha
madhara yake kwa kushirikiana na asasi binafsi. Madhara yake ni
makubwa kwa sababu yanachangia pia maambukizi ya ugonjwa wa Ukimwi,”
alisema Magata.
Kaimu Kamanda wa Polisi Mkoa wa
Iringa, Peter Kakamba, alisema kwamba, jeshi lake linajitahidi kupambana
na matumizi na biashara ya dawa hizo za kulevya, kwa kushirikiana na
jamii kupitia Ulinzi Shirikishi.
No comments:
Post a Comment