• Breaking News

    Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...

    It's more about music industry and social issues in and out of bongo land

    Tuesday, December 25, 2012

    LEO NI SIKUKUU YA KUZALIWA MWOKOZI YESU




    Krismasi (pia Noeli) ni sikukuu ambako Wakristo husheherekea kuzaliwa kwake Yesu Kristo zaidi ya miaka 2000 iliyopita. Kwa kawaida husheherekewa tarehe 25 Desemba katika Ukristo wa magharibi na tarehe 6 Januari katika ule wa mashariki.
    Historia ya Krismasi
    Tarehe halisi ya kuzaliwa kwake Yesu haijulikani kwa sababu utamaduni wa Wayahudi wa wakati ule haukuwa na sherehe au kumbukumbu ya siku ya kuzaliwa.
    Lakini baadaye Ukristo ulienea katika Dola la Roma na kati ya mataifa yaliyokuwa na kawaida ya kuzingatia siku ya kuzaliwa. Hivyo ilijitokeza hamu ya kusheherekea pia sikukuu ya kuzaliwa kwake Kristo. Ndiyo asili ya Sikukuu ya Krismasi.
    Tangu mwanzo wa karne ya 3 BK kuna kumbukumbu ya waandishi mbalimbali waliojadili tarehe ya kuzaliwa kwake Yesu Kristo.
    Habari za kwanza kabisa za makadirio ya tarehe ya kuzaliwa kwake Yesu zinapatikana kutoka Misri mnamo mwaka 200. Mwandishi Mkristo Klemens wa Alexandria (kitabu cha Stromateis I, xxi) alilalamikia udadisi wa wataalamu kadhaa wa Misri waliodai kwamba wamekadiria tarehe hiyo katika mwezi Mei, wengine katika Aprili. Alisema pia kuwa kikundi cha Kikristo cha wafuasi wa Basilides huko Misri walisheherekea Epifania pamoja na kuzaliwa kwake Yesu tarehe 6 Januari.
    Labda kadirio la tarehe ya Desemba 25 pia lina asili katika Misri. Kuanzia mwaka 200 (kwa mara ya kwanza katika maandishi ya Sixtus Julius Africanus) tunasikia kwamba wataalamu wa Misri walifikiri tarehe 25 Machi ilikuwa tarehe ya kufa kwake Kristo na pia siku ya kuzaliwa kwake. Kwa kuongeza miezi tisa ya mimba inajitokeza 25 Desemba kama tarehe ya kuzaliwa.
    Inaonekana tarehe 25 Desemba ilijitokeza wakati huo. Kuna taarifa ya mwaka 204 kutoka Ipolito wa Roma kwamba tarehe 25 Desemba ilikuwa sikukuu ya kuzaliwa kwake Yesu Kristo.
    Wataalamu mbalimbali walidai kwamba Kanisa lilipachika sikukuu ya Kristo kwenye tarehe hiyo kwa nia ya kuchukua nafasi ya sikukuu ya jua kama mungu "Sol invictus". Lakini pengine mambo yalikwenda kinyume, yaani kwamba Makaisari walianzisha sikukuu hiyo halafu wakaipanga tarehe ya Krismasi ili kushindana na Ukristo uliokuwa bado chini ya dhuluma.
    Aliyeingiza sikukuu ya Kuzaliwa Jua (Mitra) huko Roma ni Eliogabalus (kaisari kuanzia 218 hadi 222). Baadaye Aurelianus akaithibitisha rasmi mwaka 273, hatimate ikahamishiwa tarehe 25 Desemba. Wakati wa Licinius (308-324) sikukuu hiyo ilikuwa ikiadhimishwa bado tarehe 19 Desemba. (Taz. maandishi yaliyotajwa na Allan S. Hoey katika ukurasa 480 (rejeo 128) wa Official Policy towards Oriental Cults in the Roman Army, Transactions and Proceedings of the American Philological Association (70) 1939, pp 456-481).
    Kutoka Roma, uliokuwa mji mkuu wa Dola la Roma, sherehe ya 25 Desemba ilienea kote katika Ukristo.
    Wakristo wengi husheherekea tarehe 25 Desemba (Wakatoliki, Waprotestanti, sehemu ya Waorthodoksi). Kati ya Waorthodoksi kuna tarehe nyingine, hasa 6 Januari kutokana na tofauti katika kalenda.
    Habari za Krismasi katika Biblia
    Habari za Krismasi kama sherehe hazipatikani katika Biblia kwa sababu zilizotajwa hapa juu.
    Lakini hasa vitabu viwili vya Agano Jipya vina habari za kuzaliwa kwake Yesu, yaani Injili za Mathayo na Luka.
    Katika Injili ya Mathayo
    Mathayo anasimulia habari hizo katika mlango wa kwanza kuanzia aya 18 na katika mlango wa pili.
    Bikira Maria alipata mimba wakati alipokuwa mchumba wa Yosefu. Yosefu alitaka kumwacha lakini aliambiwa na malaika aanze kuishi naye na kumkubali mtoto kama wake kwa kumpa jina "Yesu".
    Mamajusi kutoka mashariki waliwatembelea na kuwaletea zawadi kwa sababu waliona nyota ya pekee iliyokuwa kwao alama ya kuzaliwa kwa mfalme mpya katika Uyahudi ikawaongoza hadi Yerusalemu. Lakini walipompitia mfalme Herode Mkuu, huyo alikasirika akimwogopa mfalme mpya. Hata hivyo aliwaelekeza Bethehemu kadiri ya utabiri wa nabii Mika.
    Yosefu alipata tena ujumbe kutoka kwa malaika akaondoka na mtoto na Maria kukimbilia Misri kabla ya askari wa Herode hawajaweza kumuua Yesu.
    Baada ya kifo cha Herode walirudi kutoka Misri lakini hawakuenda tena Bethlehemu bali kuhamia Nazareti katika mkoa wa Galilaya.
    Katika Injili ya Luka
    Katika taarifa ya Luka (mlango wa 1 na 2) Maria alipokea huko Nazareti ujumbe wa malaika mkuu Gabrieli kwamba atapata mimba na mtoto wa pekee.
    Yosefu na Maria walikwenda Bethlehemu kwa sababu ya sensa iliyowataka kwenda katika mji alikotokea Yosefu. Hapo Yesu alizaliwa katika hori la kulishia wanyama; wachungaji mabondeni walitangaziwa na malaika habari hiyo wakaja kumwona mtoto.
    Baada ya kuzaliwa wazazi walimpeleka Yesu Yerusalemu katika hekalu kufuatana na sheria ya Agano la Kale (Kitabu cha Kutoka 13,2; 13,15) halafu wakarudi kwao Nazareti.
    Habari za Krismasi katika Korani
    Korani pia ina habari za kuzaliwa kwake Yesu (nabii Isa).
    Sura ya tatu (Al Imran, 42-47) ina habari za tangazo la malaika kwa Bikira Mariamu zinazofanana na Luka 1.
    Sura ya 19 (Mariamu, 16-34) inarudia tangazo la malaika kwa Mariamu na inasimulia kuzaliwa kwake Yesu chini ya mti wa mtende, halafu majadiliano kati ya Mariamu na ndugu zake. Mtoto mchanga Yesu akaanza kusema wakati wa kuzaliwa akimtetea mama yake dhidi ya ndugu zake.
    Krismasi katika maisha ya binadamu
    Watu wote ni wakosefu na kujenga mazingira maovu hata wanayakinai na kutamani wamuone mtu tofauti, yaani mwema na mtakatifu. Pengine wanadhani fulani ni mwema kabisa, kumbe siyo.
    Haja hiyo inaturudia sisi: kwa nini nisiwe mimi mtu wa namna hiyo? Kwa nini nisianze na moja kama kwa kuzaliwa upya kabla sijawadai wengine? Zaidi tena, haja kuu ya binadamu ni kumuona Mungu mwenyewe: lakini wapi, lini, namna gani?
    Krismasi katika liturujia
    Kama kawaida, imani na liturujia ya Kikristo zinaitikia haja za binadamu. Kipindi cha Noeli kinatimiza haja tulizozitaja, kwa kuwa anazaliwa mtu mpya kabisa ambaye anatuvutia kwa wema wake na ambaye tukimuona tumemuona Mungu, tena tukimpokea tunazaliwa upya kama wana wa Mungu.
    “Leo amezaliwa kwa ajili yenu Mwokozi, ndiye Kristo Bwana”. Tunapoadhimisha Noeli tangazo hilo la malaika kwa wachungaji linatufikia sisi. Si kujidanganya, kana kwamba Yesu angezaliwa leo, wala hatukumbuki tu tukio la zamani, bali fumbo la kuzaliwa Bwana linatufikia leo katika liturujia na kutuletea neema zake. Hivyo tunaweza tukazaliwa upya kwa kushiriki kuzaliwa kwa kichwa chetu.
    Liturujia inashangilia hivi, “Lo! Mabadilishano ya ajabu! Mwana wa Mungu anakuwa mtu kusudi mtu awe mwana wa Mungu!”. Tena si binadamu tu, bali viumbe vyote vinapata heshima mpya kwa Neno wa milele kujifanya kiumbe.
    IMEANDALIWA NA JOHNSON JABIR KWA MSAADA WA MTANDAO

    No comments:

    3500K