Wachezaji
17 wa timu ya Taifa ya vijana wenye umri chini ya miaka 17 (Serengeti Boys)
wamefanyiwa vipimo vya kubaini umri wao halisi (MRI Tests) kwenye hospitali ya
Aga Khan, Dar es Salaam.
Upimaji huo ulifanyika Julai 14
mwaka huu chini ya usimamizi wa mjumbe wa Kamati ya Tiba ya Shirikisho la Mpira
wa Miguu Afrika (CAF), Dk. James Sekajugo kutoka Uganda
na Mwenyekiti wa Kamati ya Tiba ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania
(TFF), Dk. Sylvester Faya.
Dk. Sekajugo alisema vipimo hivyo
vya Magnetic Resonance Imaging (MRI) vinafanya kutokana na maelekezo ya CAF kwa
nchi zote ambazo zitashiriki mashindano ya U17 ambayo fainali zake zitafanyika
mwakani nchini Morocco
ili kubaini umri halisi wa wachezaji hao.
Amesema vipimo vya MRI havina
madhara kama ilivyo kwa X-ray ambapo vyenyewe
vinachunguza uimara wa mifupa ili kubaini umri halisi wa mchezaji, na uwezo
wake ni kubaini watu walio chini ya umri wa miaka 17.
CAF imeamua vipimo hivyo vifanyike
kabla ya wachezaji kuingia kwenye mashindano kwani Afrika inakabiliwa na tatizo
sugu la kudanganya umri wa wachezaji.
Amesema uamuzi wa CAF kufanya vipimo
vya MRI kabla ya wachezaji kuanza mashindano umelenga kuhakikisha wachezaji
wanaoshinda wana umri sahihi, badala ya vipimo hivyo kufanyika wakati wa
fainali.
Naye Dk. Faya ambaye pia ni mjumbe
wa Kamati ya Utendaji ya TFF amesema wachezaji 10 waliobaki watafanyiwa vipimo
hivyo baadaye kabla ya mechi ya michuano hiyo CAF dhidi ya Kenya itakayochezwa Septemba mwaka
huu.
Wachezaji tisa wako nchini Burundi
kwenye michuano ya Rolling Stone Multipurpose Acre Foundation wakati mmoja
(Dickson Ambundo) amekwenda Ujerumani na timu ya TASC ya Mwanza.
Walioko Burundi ni Hamad Juma, Mgaya
Jaffar, Ismail Gambo, Mohamed Hussein, Hussein Ibrahim, Mudathir Abbas, Farid
Shah, Joseph Lubasha na Kelvin Friday.
Dk. Faya amesema vipimo vya MRI
kupanywa mapema ni vizuri kwa sababu tatizo la udanganyifu wa umri lipo, lakini
pia litaisaidia TFF kwani inatumia gharama kubwa kuandaa timu, hivyo ni vizuri
ikaandaa timu ya wachezaji wenye umri sahihi badala ya waliodanganya umri ambao
hawataruhusiwa kushiriki mashindano.
Mwaka 2005 Serengeti Boys ilifuzu
kucheza fainali za Afrika zilizofanyika Banjul,
Gambia lakini
ilinyang’anywa nafasi hiyo baada ya kubainika kuwa baadhi ya wachezaji wake
walikuwa wamezidi umri wa miaka 17.
No comments:
Post a Comment