• Breaking News

    Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...

    It's more about music industry and social issues in and out of bongo land

    Friday, June 8, 2012

    Dawa Za Kulevya Zaitikisa Iringa




             BIASHARA ya dawa za kulevya imeshika kasi mkoani Iringa huku vigogo kadhaa wakitajwa kuhusika, Kwanza Jamii-Iringa linaripoti.
          Taarifa zinaeleza kwamba, wafanyabiashara kadhaa maarufu mkoani humo wanatajwa kujihusisha katika usambazaji na utumiaji wa dawa hizo, hususan cocaine, heroin na Mandrax.
           Kundi rika la vijana wenye umri kati ya miaka 18 na 35 ndilo linaloongoza kwa biashara hiyo kwa utumiaji na usambazaji, huku bhangi ikiwa inaongoza miongoni mwa orodha ya dawa za kulevya.
    “Huwezi kuipiga vita biashara ya dawa za kulevya ikiwa vigogo wenyewe ndio wanaosambaza na kutumia. Wapo wanajulikana, lakini hatujui ni kwa vipi serikali inashindwa kuwakamata,” kimeeleza chanzo chetu cha habari.
    Inaelezwa kuwa, wafanyabiashara kadhaa wa mjini humo, ambao baadhi wanadaiwa kuwemo kwenye orodha ya vigogo 58 wa dawa za kulevya iliyopelekwa kwa Rais Jakaya Kikwete mwaka 2006, ndio miungu-watu wanaojificha kwenye mwavuli wa biashara zao halali pamoja na kusaidia jamii.
          Taarifa zinaeleza kwamba, vigogo wengi na hasa wenye fedha, ndio watumiaji wakubwa wa dawa za viwandani kama heroin na cocaine kwa vile hawawezi kwenda kununua bhangi mitaani kutokana na hadhi zao, huku kundi kubwa la vijana likitajwa kutumia zaidi bhangi.
    Wananchi kadhaa waliohojiwa na gazeti hili kwa masharti ya kutotajwa majina yao, walisema matumizi ya dawa za kulevya mkoani humo yanazidi kushika kasi licha ya serikali kusema yamepungua.
              “Huku mitaani sisi ndio tunaowaona watumiaji, wanaongezeka kila wakati na hakuna juhudi za kuwapunguza, hasa vijana ambao wanazidi kuathirika na matumizi hayo,” walisema wananchi hao.
    Kauli hiyo ya kukithiri kwa matumizi ya dawa za kulevya iliungwa mkono na Ofisa Mtendaji wa Kata ya Kitanzini iliyo katikati ya Manispaa ya Iringa, Raphael Magata, ambaye alisema matumizi ya dawa za kulevya kwa vijana yanazidi kuongezeka.
    Magata alisema kwamba, pamoja na juhudi kubwa zinazofanywa na serikali pamoja na asasi mbalimbali za kijamii kuelimisha juu ya madhara yake, lakini idadi ya vijana wanaojihusisha na biashara hiyo inazidi kuongezeka, hivyo kuitaka jamii ishiriki kupambana ili kuokoa nguvu kazi isipotee.
    “Vijana wengi hivi sasa wanajihusisha na utumiaji wa dawa za kulevya ingawa serikali inajitahidi kuwalimisha madhara yake kwa kushirikiana na asasi binafsi.     Madhara yake ni makubwa kwa sababu yanachangia pia maambukizi ya ugonjwa wa Ukimwi,” alisema Magata.
          Kaimu Kamanda wa Polisi Mkoa wa Iringa, Peter Kakamba, alisema kwamba, jeshi lake linajitahidi kupambana na matumizi na biashara ya dawa hizo za kulevya, kwa kushirikiana na jamii kupitia Ulinzi Shirikishi.

    No comments:

    3500K