NI NYUMBA, KUTA ZA MABILIONI ZILIZOJENGWA UFUKWENI, MMOJA AKIMBILIA KORTINI KUZUIA JUMBA LAKE LA SH1.5 BILIONI Geofrey Nyang’oro SERIKALI
jana ilikunjua makucha yake kwa vigogo waliojenga nyumba za kifahari
kando ya Mito ya Mbezi Beach, Mndumbwe na eneo la Hifadhi ya Mikoko, Dar
es Salaam baada ya kuzibomoa katika operesheni iliyosimamiwa na Kikosi
cha Kutuliza Ghasia (FFU) cha Jeshi la Polisi.
Hiyo ni sehemu ya
utekelezaji wa tamko la Makamu wa Rais la mwaka 2004 ambalo lilitaja
maeneo tengefu ambayo yalipaswa kuhifadhiwa zikiwamo fukwe za bahari
ambazo zina mikoko ambayo ni mazalia ya samaki baharini. Licha ya tamko
hilo na sheria mbalimbali, bado maeneo ya fukwe za bahari yamekuwa
yakivamiwa.
Katika kusimamia sheria na tamko hilo, Wizara ya
Maliasili na Utalii, Kitengo cha Hifadhi ya Misitu, Baraza la Taifa la
Kuhifadhi Mazingira (NEMC) na Halmashauri ya Manispaa ya Kinondoni,
ziliamua kuratibu bomoabomoa hiyo ya nyumba za kifahari zilizojengwa
maeneo tengefu ya bahari.
Bomoabomoa hiyo ambayo iliendeshwa
chini ya ulinzi mkali wa polisi wa FFU chini ya Kamanda wa Polisi Mkoa
wa Kinondoni, Charles Kenyela na kwa mujibu wa Mkurugenzi wa Uzingatiaji
na Utekelezaji wa NEMC, Dk Robert Ntakamulenga, jumla ya nyumba 27 kati
ya hizo 15 zikiwa zimekamilika ujenzi, nane uzio (fence) na nyingine
katika hatua za awali za ujenzi, zilibomolewa.
Kazi ya kubomoa
nyumba hizo iliyofanywa na kampuni ya Majembe Auction Mart, ilianza huku
wakazi wa nyumba hizo wakiwekwa chini ya ulinzi mkali wa FFU na polisi
wengine waliokuwa wamesheheni mabomu ya machozi, bunduki na gari la
kumwaga maji ya kuwasha.
Bomoabomoa hiyo ilianzia katika eneo la
Hifadhi ya Mikoko, Mbezi Beach mnamo saa 2:00 asubuhi na watu waliokuwa
wakiishi katika nyumba hizo walilazimika kutoa vitu vyao nje huku
kububujikwa machozi.
Mmoja wa wakazi wa eneo hilo na Mchungaji wa
Kanisa la Dar es Salaam Christian, George Makala alisema kitendo hicho
kinasikitisha kwa kuwa muda uliotolewa kwao ni mdogo na wasingeweza
kujiandaa kuhama.
Akizungumzia tukio hilo muda mfupi baada ya
kubomolewa nyumba yake na kanisa hilo, Mchungaji huyo alisema kitendo
hicho hakikufuata taratibu na kimesababisha hasara ya mali nyingi kwa
wakazi wa eneo hilo akisema kama wangeachwa wahame zingeokolewa.
“Ninasikitika
sana kwani kitendo hiki hakikufuata taratibu, alikuja Waziri wa Nyumba,
Ardhi na Makazi Profesa Anna Tibaijuka, Mbunge wetu, Halima Mdee na
Meya wa Manispaa ya Kinondoni, Yusuf Mwenda wakatuambia eneo hilo siyo
la hifadhi, bali ni hatarishi, sisi tuliwaambia tuna uwezo wa
kukabiliana nalo ndipo waziri aliposema atatoa tamko,” alisema Mchungaji
Makala na kuongeza:
“Tukiwa tunasubiri tamko kutoka kwa waziri
na vibali tunavyo, tumeshangaa (juzi) Jumapili tunaamka na kukutana
alama za X. Hatukujua nani ameweka, leo (jana) ghafla tunashangaa
tingatinga zimekuja na kubomoa.”
Alisema walichofanyiwa siyo haki
kwa sababu hawakupewa muda wa kujiandaa kutafuta mahali pa kuhamia
lakini pia wangebomoa nyumba zao kuokoa mali zao. “Kwa sasa
tutawasiliana na mwanasheria wetu kuona kama kuna uwezekano wa kuchukua
hatua ili twende mahakamani, lakini hilo litategemea nini mwanasheria
atatushauri,” alisema Makala.
Wananchi washangilia Wakati
Mchungaji Makala akielekeza kilio chake kwa waratibu wa shughuli hiyo,
baadhi ya watu waliofika kushuhudia tukio hilo waliisifu Serikali
wakisema sheria sasa imeanza kufanya kazi. Mmoja wa wakazi hao,
Samuel Laizer alisema kilichofanywa sasa na Serikali kinaonyesha kuwa
sasa inafanya kazi na hakutakuwa na mtu atakayekuwa juu ya sheria. “Tukio
hilo limenifurahisha sana, tumezoea kuona Serikali ikituonea sisi
maskini, lakini kitendo cha kubomoa nyumba hata za vigogo waliovunja
sheria, sasa tunaamini watu wote tutakuwa sawa,” alisema Laiser.
Katika
eneo la Mto Mbezi Beach, kikosi hicho cha ubomoaji kilivunja kuta
kadhaa zilizokuwa zimezungushwa katika viwanja saba vilivyokuwa karibu
na mto huo pamoja na Mto Mndumbe inayomwaga maji katika Bahari ya Hindi.
Mwanasheria
wa NEMC, Manchare Heche alisema baadhi watu wanaomiliki viwanja hivyo
waliendelea kujenga majumba ya kifahari licha ya zuio hilo lilitolewa
zaidi ya mara tatu.
Heche pia alisema bomoabomoa hiyo ilikuwa
iikumbe moja ya nyumba ya kifahari katika Mto Mbezi lakini mmiliki wake
ameweka pingamizi katika Mahakama Kuu Kitengo cha Ardhi. Kwa mujibu wa
watu waliokuwa katika eneo hilo, nyumba hiyo inakadiriwa kuwa na thamani
ya Sh1.5 bilioni.
Akizungumzia shughuli hiyo ya jana, Kaimu
Mkurugenzi Usimamizi Rasilimali na Wakala wa Huduma za Misitu, Zawadi
Mbwambo alisema kazi hiyo imechelewa kutokana na kuhusisha idara, wizara
na taasisi tofauti katika utendaji wake.
Alisema kazi hiyo
itakuwa endelevu na itawahusu watu wote waliojenga katika maeneo ya
fukwe za bahari na kusisitiza kuwa umbali unaoruhusiwa kujenga nyumba
kutoka eneo la bahari ni meta 60.
Kwa upande wake, Dk
Ntakamulenga alisema kazi hiyo ya kubomoa nyumba katika maeneo ya
hifadhi za taifa, fukwe za bahari na kando ya mito ni endelevu na akatoa
wito kwa watu wote waliojenga katika maeneo hayo kuchukuka tahadhari
mapema kuondoa usumbufu. “Tumechelewa kuchukua hatua kutokana na
zoezi hili kushirikisha mamlaka zaidi ya mmoja, tulikutana kujadili na
kuona umuhimu wa kuunganisha nguvu ili utekelezaji wake usiingilie
mamlaka nyingine,” alisema Dk Ntakamulenga.
Alisema kazi hiyo
pindi itakapomalizika katika jiji la Dar es Salaam ambako kuna viwanja
zaidi ya 100, vinavyopaswa kurudishwa katika mamlaka husika, itahamia
mikoani na itawahusu pia watu wote waliojenga nyumba zao kwenye hifadhi
za taifa, kando ya mito na kwenye fukwe za bahari kitendo
kinachosababisha uharibifu wa mazingira.
Polisi Kinondoni yatoa onyo Kamanda
Kenyela aliwataka watu wote waliojenga nyumba zao katika maeneo
yanayokatazwa na Serikali, kuzibomoa wenyewe ili kukwepa mkono wa
sheria.
“Tukio la leo ni kwamba tumewasha taa, sasa watu wote
waliojenga nyumba zao kinyume na sheria katika jiji la Dar es Salaam na
hata wenye migogoro ya ardhi ambao Mahakama ilishatoa hukumu ni vyema
wakabomoa wenyewe, watii sheria pasipo shuruti,” alisema.CHANZO MWANAINCHI |
No comments:
Post a Comment