WENYEVITI wa vyama vya Chadema, NCCR Mageuzi na CUF
wameiponda Bajeti ya Serikali ya mwaka wa fedha 2012/2013 iliyowasilishwa
bungeni jana na Waziri wa Fedha, Dk William Mgimwa wakisema imeongeza mzigo kwa
walipa kodi kutokana na gharama kubwa za uendeshaji wa Serikali.
Wakizungumza
kwa nyakati tofauti baada ya kuwasilishwa kwa bajeti hiyo jana, wenyeviti hao
walisema hakuna matumaini kwa Watanzania kupitia Bajeti hiyo kwani fedha nyingi
zimerundikwa kuwanufaisha wachache huku umma ukiambulia patupu.
Mwenyekiti wa Chadema,
Freeman Mbowe alisema: “Hakuna mkataba wa makusudi wa kupunguza matumizi ya
Serikali, ahadi yake ya kupunguza matumizi kwa kupunguza posho zisizo na tija
na matumizi mengine haikutekelezwa.” Mbowe ambaye pia ni Kiongozi wa Kambi ya
Upinzani Bungeni, amesema ameshangazwa na kutokuwapo kwa nyongeza ya mishahara
kwa watumishi wa umma na badala yake fedha nyingi kurundikwa katika matumizi ya
kawaida ya Serikali. Kwa upande
wake, Mwenyekiti wa CUF, Profesa Ibrahim Lipumba alisema matatizo makubwa
katika bajeti hiyo ni kutengwa kwa fedha kidogo za maendeleo na kwamba
kinachoshangaza ni Serikali kushindwa hata kugharimia matumizi ya kawaida. Mwenyekiti wa
NCCR Mageuzi, James Mbatia alisema Serikali lazima ijifunze kubadilika kwani
kilichotangazwa jana kwenye Bajeti yake ni marudio ya miaka yote.
Mbunge wa
Simanjiro (CCM), Christopher Ole Sendeka amesema Bajeti hiyo kama
zilivyo nyingine, imeendelea kujikita katika kuongeza kodi katika bidhaa
zilezile kila mwaka. Mbunge wa Viti Maalumu (CCM), Ester Bulaya amesema Bajeti
hiyo ni nzuri akipongeza mkakati wa ukarabati mkubwa wa Reli ya Kati.
No comments:
Post a Comment