Msanii
wa filamu ambaye pia ni Mkurugenzi wa Kituo cha Mafunzo ya Filamu
cha Tanzania Film Training Centre (TFTC) Emmanuel Myamba maarufu
kama Pastor Myamba akiwasilisha mada kwenye Jukwaa la Sanaa wiki
hii. Kushoto kwake ni Katibu wa Shirikisho la Filamu nchini Wilson
Makubi
Na Mwandishi Wetu
Wadau
wa Sanaa wamehoji uhalali wa wasanii wa filamu kutumia kiingereza
kwenye majina ya filamu zao huku wakishangazwa na kazi hizo kubeba
maudhui ya kizungu zaidi.
Wakizungumza
wiki hii kwa nyakati tofauti kwenye programu ya Jukwaa la Sanaa, wadau
hao walishangazwa kitendo cha filamu hizo kutumia majina ya kizungu
wakati hapa kwetu kuna filamu nyingi kutoka nje zinazotumia lugha za
kihindi, kichina, kifaransa na zinafanya vizuri.
“Hoja
kwamba, wanatumia majina ya kiingereza ili kuteka soko la kimataifa ni
ya kitoto, mbona hapa kwetu kuna filamu nyingi za kihindi na kichina
zinanunuliwa kwa wingi? Hapa kuna udhaifu katika kutengeneza filamu
zenye ubora tujikite huko”alisema Mzee Nkwama Bhallanga.
Kwa
mujibu wa wadau wengi waliozungumza, filamu ni taaluma inayozungumza
kwa kutumia picha na vitendo zaidi hivyo haihitaji mtazamaji kufahamu
lugha iliyotumiwa ili afahamu maudhui na ujumbe unaowasilishwa na kazi
husika ya filamu.
“Maneno
kwenye filamu si muhimu sana, kinachozungumza ni matendo na picha
zaidi, ndiyo maana kuna watu wanaangalia picha za Kikorea na
wanaburudika na kuelewa kinachoendelea” alisema Godfrey Lebejo ambaye ni
Murugenzi wa Idara ya Utafiti, Mafunzo na habari, BASATA.
Aliongeza
kuwa, kinachoitesa tasnia ya filamu kwa sasa ni kukosekana kwa weledi
na uhalisia wa tamaduni zetu kunakosababishwa na wimbi kubwa la watu
kujiingiza kwenye filamu ili kufanikisha mambo yao yaliyo nje ya maadili
na utamaduni wetu.
“Inawezekana
vipi utengeneze filamu ambayo baba, mama na watoto hawawezi kukaa
pamoja kuitazama? Tufike mahali tuseme mambo haya ya kipuuzi basi kwenye
filamu zetu” alionya Lebejo.
Awali akiwasilisha mada kuhusu Filamu, wasanii na haja ya kujiendeleza kielimu, Msanii
wa filamu Emmanuel Myamba maarufu kam Pastor Myamba alisema kuwa,
tasnia ya filamu inakosa weledi hivyo kuhitaji mabadiliko.
“Ni
wazi ukiangalia filamu zetu zinakosa weledi katika uandishi wa miswada,
uongozaji, uhariri na hata uumbaji wa wahusika. Lazima tukubali udhaifu
huu turekebishe” alisema Myamba ambaye kwa sasa amefungua kituo cha
mafunzo ya filamu kiitwacho Tanzania Film Training Centre (TFTC)
kilichoko Ubungo.
No comments:
Post a Comment